Kilichomwangusha Sumaye chatajwa

SIASA za makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimetajwa kuwa chanzo cha kuangushwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kupitia Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara. Sumaye ambaye anatajwa kuwa ana nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, alishindwa na Dk Mary Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji). Katika uchaguzi huo, Sumaye alipata kura 481 dhidi ya Nagu, aliyepata kura 648. Mbali na Sumaye, wajumbe wengine waliokuwa wakimuunga mkono akiwamo Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Goma Gwantu, pia walishindwa katika uchaguzi huo. Dalili za kushindwa kwa Sumaye, ambaye alikuwa akiungwa mkono na wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM wa wilaya hiyo, zilianza kuonekana wiki moja kabla ya uchaguzi huo. Kambi ya Dk Nagu ambayo inatajwa kwamba inaungwa mkono na kambi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, ilionekana kuwa na “ushawishi” mkubwa katika vikao vya kamati ya siasa ya mkoa na kwenye Kamati Kuu ya CCM. Hali hiyo, ilitokana na ukweli kuwa Dk Nagu kama taratibu ambazo zilihitajika, hakupewa baraka na kamati ya siasa ya wilaya hiyo, kugombea kwa kile ambacho kilielezwa kukwepa mpasuko wa CCM Hanang’ na pia kumpa heshima Sumaye. Hata hivyo, habari zimeeleza kuwa tofauti na msimamo wa Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo, Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara, ilionekana kumuunga mkono Dk Nagu hasa kutokana na ukweli kuwa karibu nusu ya wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wagombea. Kikao cha kamati ya siasa ya mkoa, licha ya kurejesha jina la Dk Nagu pia, kilipendekeza kuondolewa majina ya wagombea kadhaa katika wilaya ya Hanang’ likiwamo jina la Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Goma Gwaltu ambaye alikuwa kambi ya Sumaye. Taarifa za kupendekezwa kuondolewa majina ya wanaomuunga mkono Sumaye, zilitolewa na baadhi ya wajumbe wa Wilaya ya Hanang’, lakini hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndeng’aso Ndekubali alizikanusha. “Kamati ya siasa ya mkoa ni kikao cha siri na nadhani ni mapema mno kulalamikia suala hilo, ni vyema wakasubiri uamuzi wa juu, ” alisema Ndekubali. Hata baada ya kurejeshwa majina na Nec, ilibainika kuwa wagombea ambao Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, iliwapa alama za chini, wamerejeshwa katika mchakato wa uchaguzi. Dalili za kuanguka Sumaye, pia zilijionyesha siku ya kupiga kura, ukumbini na nje ya ukumbi kutokana na wajumbe waliokuwa wanamuunga mkono Dk Nagu kuwa na uhakika mkubwa wa ushindi. Wakati wa kujieleza ili aombe kura, Sumaye ambaye alionekana kama tayari amebaini nguvu ya Dk Nagu, alieleza kushangazwa na uamuzi wa Dk Nagu kugombea nafasi hiyo, hali ya kuwa ni waziri. Sumaye, pia alikemea kile alichodai kuwa ni rushwa kwenye chaguzi za CCM na kuahidi kama akichaguliwa, angeshirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha anawachukulia hatua kali watoa rushwa. Awali Dk Nagu katika maelezo yake, alitumia fursa ya kuomba kura kukanusha kuwa anatumiwa na kundi la Lowassa ili kumkwamisha Sumaye. Dk Nagu alifafanua kuwa yeye kama Mbunge wa Hanang’ na Waziri, kamwe hawezi kutumiwa na kundi fulani kwa masilahi ya makundi kwani hata yeye ana sifa za kuchaguliwa. Wakati wa maswali, Dk Nagu hakuulizwa wakati Sumaye aliulizwa maswali matatu ambayo aliyajibu kwa ufasaha, lakini hakuchaguliwa. Mwenyekiti wa CCM aliyeshindwa, Goma Gwaltu, alieleza kupinga mambo kadhaa yaliyokiukwa katika uchaguzi, lakini hata hivyo, alisisitiza kujiandaa kutoa tamko rasmi. “Nitazungumza siku si nyingi kuelezea uchaguzi huu,” alisema Gwaltu. Naye Sumaye kwa upande wake, alisema anakusudia kuzungumzia yaliyojiri katika uchaguzi huo hivi karibuni.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: